TAPO Logo

TAPO Logo

Sunday, April 11, 2010

Gombe watakiwa kushirikisha wananchi

Leonard Mubali, Kigoma

KAMATI ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, imeushauri uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe, mkoani Kigoma, kushirikisha wananchi katika mpango wa upanuzi wa hifadhi hiyo, ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.


Hifadhi hiyo inahitaji eneo zaidi, kwa ajili ya kuboresha ikolojia ya sokwe na upanuzi wa huduma za kitalii.


Ushauri huo ulitolewa juzi na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Raphael Mwalyosi, alipokuwa akichangia hoja kuhusu mpango wa kupanua eneo la hifadhi hiyo.


Profesa Mwalyosi alisema mpango huo ni mzuri, lakini lazima kwanza uongozi wa hifadhi, uwashirikishe wananchi wanaoishi jirani na hifadhi, ili kuepuka migongano kati ya pande hizo mbili.


Alisema vitendo vya kutowashirisha wananchi katika kuchukua maeneo kwa ajili ya upanuzi wa hifadhi, vimesababisha migongano isiyokuwa ya lazima, kama ilivyowahi kutokea katika baadhi ya maeneo hapa nchini.


Alisema kwa msingi huo, kuna haja kwa uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe, kuepuka hilo, ili kuwa katika nafasu mzuri ya kuendeleza uhusiano kati yake na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi.


Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Noella Myonga, hifadhi hiyo inaomba kuongeza eneo la kilometa 31, ili hatimaye kuifanya iwe na ukubwa wa kilometa 83 za mraba.


Myonga alisema hata hivyo, eneo linaloombwa si la makazi ya watu na kwamba ni la ufukwe wa Ziwa Tanganyika, ambalo uongozi unaamini kuwa, halitakuwa na mlolongo mrefu kuhusu fidia.


Alisema kuongezwa kwa eneo hilo, kutasaidia kuongeza ikolojia ya hifadhi, vivutio zaidi ya sokwe na kuwafanya watalii kufurahia.


Pia alisema kama eneo hilo litahifadhiwa kikamilifu, usalama wa mazalia ya samaki ambayo kwa sasa, yanaharibiwa na wavuvi, utakuwa mkubwa.


Myonga alisema hatua hiyo pia itasaidia kudhibiti watu wanaoishi karibu na Hifadhi ya Gombe, kupita katika eneo hilo kwa njia za miguu, jambo ambalo ni la hatari kwa maisha ya sokwe, hasa ikizingatiwa kuwa wanaweza kuambikizwa kwa urahisi, magonjwa ya binadamu.


Kuhusu ikama ya wafanyakazi wa hifadhi, ilielezwa kuwa imepungua, lakini hatua zinachukuliwa kuhakikisha kuwa pengo hilo linazibwa mapema.

Nani ataiokoa Idara ya Wanyamapori?

Nani ataiokoa Idara ya Wanyamapori?



Kulwa Karedia




TUNAKUTANA tena katika safu hii nikiamini wazi kuwa sote tu wazima wa afya njema na wale ambao hali si nzuri nawaombea kwa Mungu awatie nguvu haraka.
Leo nakutana nawe kama ilivyo ada, kujadili masuala mbalimbali yanayojitokeza kwenye taifa letu ambalo tunaambiwa ni masikini sana, jambo ambalo mimi sikubaliani nalo hata kidogo.

Hivi sasa macho na masikio ya Watanzania walio wengi yanaelekezwa kwenye masuala ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Kila kona ukipita hivi sasa utasikia mtu fulani anatufaa kuwa mbunge au diwani, lakini kwenye urais huko mmmh. Tuachane na hayo, leo mada kuu katika waraka tutaigusa Idara ya Wanyamapori.

Moja ya sekta ambayo imekuwa nguvu kuu ya uchumi wa Tanzania ni sekta ya utalii wa ndani ambao kwa mapenzi mema Mungu alilibariki taifa hili kuwa na vivutio vya kila aina.

Alibariki kuwepo wanyama wa aina mbalimbali, milima, madini, ziwa lenye kina kirefu na vingine vingi, kwa hayo tunasema asante.

Lakini pamoja na Mungu kutupatia wanyama na vitu vingine kwa ajili ya faida ya taifa na watu wake, hali inaonekana kwenda kombo kutokana na ukweli uliopo kuwa matumizi yake yamekuwa ni hatari kwa kundi la watu wachache.

Idara ya Wanyamapori Tanzania ambayo iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ‘kichaka cha watu wachache’ kujinufaisha huku ikiwaacha Watanzania zaidi ya milioni 40 wakikosa fursa ya kunufaika na rasilimali za taifa.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tatu ilipoingia madarakani kumekuwa na kelele nyingi kuwa sekta hiyo imekuwa moja ya sehemu ambayo watu au viongozi wanaoteuliwa kuiongoza wamekuwa miungu watu.

Mbali ya kuwa ‘miungu watu’ wamegeuza sekta hiyo kuwa ‘kitega uchumi’ kikuu kwa kushirikiana na watu fulani fulani wanaotoka nje kwa ajili ya biashara ya kuuza meno ya tembo, wanyama kusafirishwa nje ya nchi au kuuawa kwa wingi, hilo kwao ni jambo lisilo wakosesha usingizi hata kidogo.

Wiki hii wasamaria wema na wazalendo waliamua kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kuelezea unyama na umafia unaofanywa na vigogo kadhaa wa idara hiyo nchini.

Katika barua hiyo, wazalendo hao walimtaka rais achukue hatua za haraka na za makusudi ili kupunguza vitendo vya ujangili katika mapori ya Serengeti, Loliondo, Ugalla na Selous ambavyo vinatishia uhai wa baadhi ya wanyama katika mapori hayo.

“Mheshimiwa rais, hali ya wanyama katika sekta ya wanyamapori ni hatari, tembo wanawindwa kiholela na matumizi ya fedha kwa mamilioni yanaliwa na watu wachache kana kwamba serikali yako imehama Tanzania,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, wafanyakazi hao wanadai hivi sasa wawindaji majangili kutoka nchi za Korea, China, Thailand na Uarabuni ndio wamekuwa wakimaliza wanyama hao ndani ya mapori hayo.

“Pamoja na mamilioni ya fedha tele kutoka mifuko kama TWPF, fedha hizo zinaishia kwenye mifuko ya wakubwa ambao wamesheheni safari za nje ya nchi kila kukicha.

“Kwa kifupi mheshimiwa rais ili kuokoa kidogo kilichopo, baadhi ya vigogo hawa (majina tunayo) wanapaswa kung’atuka mara moja,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Baadhi ya maofisa wa wizara hiyo wamehusishwa kuwasaidia majangili kufanikisha azima ya kuhujumu wanyama hao na rasilimali nyingine za taifa.

Baadhi ya maofisa hao wanadaiwa kukwamisha jitihada za udhibiti wa vitendo hivyo zinazofanywa na serikali.

Habari zaidi zinaeleza kuwa kuna vitendo vya ujangili na utoroshaji wa nyara za taifa vimeongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni huku baadhi ya wafanyabiashara wa Kitanzania wanadaiwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa wizara hiyo kufanya vitendo hivyo.

Wafanyabiashara na maofisa hao wanadaiwa kuwa watoroshaji wakubwa wa nyara za wanyamapori kwenda Asia na Ulaya na kujipatia mamilioni ya fedha.

Uchunguzi wa kina umebaini kuwa kati ya Machi na Juni mwaka jana, tani 10,000 za pembe za wanyamapori zilisafirishwa kwenda Pakistan na Afghanistan kutoka kampuni ya mfanyabiashara mmoja.

Wafanyakazi hao, wamemlaumu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Arasimus Tarimo, kuwa amekuwa chanzo cha kushindwa kudhibiti hali hiyo.

“Nakwambia tumekuwa katika matatizo makubwa, hatuna ushirikiano na mkurugenzi huyu, hata Desemba 2009 na Januari 2010 hakuna askari aliyekwenda porini, kwani wote waligoma kutokana na madai yao ya muda mrefu. Siku tuliyokwenda porini tulikuta mauaji makubwa ya tembo, wanyama wengine na upasuaji wa mbao ovyo,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Mkurugenzi wa Wanyamapori, Tarimo, alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na madai hayo, aling’aka na kukana jina lake.

“Ndiyo, mimi ni Tarimo, hebu uliza swali lako,” alisema.

Baada ya kuulizwa kuhusu tuhuma hizo, alianza kwanza kusema: “Mimi siitwi jina hilo, niko Arusha kwa shughuli zangu,” alisema.

Tanzania Daima ilipompigia simu Tarimo tena alisema: “Nakwambia ndugu, niambie unataka nini? Mimi niko katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, narudia, sina cha kusema jamani eeeh.”

Ndugu msomaji, hayo ni machache kati ya mengi yaliyoandikwa kwenye waraka wa kwenda kwa Rais Kikwete kuhusiana na tuhuma hizo.

Ni wazi kwamba kasi ya uwindaji inayofanywa na majangili inaweza kusababisha wanyama kama tembo kutoweka kwa asilimia 45 kama hatua za makusudi na za haraka hazitachukuliwa.

Takwimu zinaonyesha kwa upande wa Tanzania akiba ya meno ya tembo ni tani 89.8, ambazo thamani yake ni sh bilioni 27.

Itakumbukwa siku ambayo Rais Kikwete alipofanya mabadiliko makubwa kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii na kumuondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo, Emmanuel Severe, mamia ya wafanyakazi wa sekta hiyo walishangilia kutokana na kulalamikiwa kwa ubabe wake.

Watu walikuwa wakijiuliza ana kinga ya aina gani kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu, kiasi cha kushindwa kung’oka katika idara hiyo ilhali alikuwa ana tuhuma lukuki? Lakini kama Waswahili wasemavyo ‘njia ndefu haikosi kona’, siku moja mambo yalitimia.

Severe alifikia hatua ya kumdhalilisha waziri wake, Anthony Diallo, kwa kukataa uhamisho, na kwa kujiamini kabisa akakaririwa akisema kuwa yeye atahamishwa na aliyemteua.

Ni ukweli ulio wazi kuwa mkurugenzi wa sasa naye ameanza ‘kuchomoa makucha yake’ kama ya mtangulizi wake, hadi inapofikia hatua ya kupigiwa simu na kukana jina lake na namba za simu za aina tatu alizonazo. Hii ina maanisha nini kwa kiongozi wa umma?

Hii ni dalili tosha kwamba eneo hili si safi wala salama, linahitaji kupigwa msasa wa haraka ili kurejesha imani kwa wafanyakazi na Watanzania.

Hivi jamani, tujiulize, hawa watawala wanapata wapi jeuri hii? Au wanashikiliwa na vigogo kadhaa kwa manufaa yao?

Nasema umefika wakati sasa, Rais Kikwete na wasaidizi wake kuonyesha makucha kwa viongozi wa aina hii, ambao wanaonekana kuwekwa kwenye sekta hizi na kujineemesha kwa manufaa yao kila kukicha.

Katika waraka wa wafanyakazi kwenda kwa Rais Kikwete, wamemtupia lawama Tarimo kwa kushindwa kuendesha idara hiyo kama inavyotakiwa, wamelalamikia wingi wa safari nje ya nchi, uhaba wa magari na mambo mengine. Nasema muda wa kupiga ‘porojo’ na viongozi wasio na faida kwa taifa umekwisha.

Tunaelewa wote jinsi viongozi wa nchi za Afrika wanavyopapatikia wakubwa (wafadhili) ambao huwaendesha jinsi wanavyotaka, tunasema hatutakubali kuona hali hii inaendelea ndani ya taifa huru kama hili.

Kwa kumalizia, nasema kitendo kilichoonyeshwa na Tarimo kwa kukana jina lake wakati anapoombwa kutoa ufafanuzi wa jambo ambalo linahusu idara yake, ni kielelezo tosha jinsi idara hiyo inavyoendeleza vitendo vya ubabe.

Pili, kitendo hicho kimeonyesha wazi Tarimo yuko pale si kwa faida ya Watanzania, bali ni kundi la watu wachache kwa manufaa yao.

Kama kweli angekuwa na uchungu wa upotevu wa mali hizi angetoa ufafanuzi ili kuisaidia serikali kupitia vyombo vya habari.

Tatu, nasema haya ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo hayakubaliki kamwe kwa jamii iliyostaarabika katika karne hii.

Tunahitaji viongozi wenye uchungu na taifa hili, si waponda raha.

Ndiyo maana nasema mzimu wa Severe bado upo Idara ya Wanyamapori, umefika wakati wa mamlaka za juu kuwa macho, tuondoe urafiki, uswahili na ushikaji kwenye masuala ya kitaifa.

Mapambano daima.